Upo Hapa: Home

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUELIMISHA JAMII JUU YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA

E-mail Print PDF

Waandishi wa habari wametakiwa kutumia taaluma yao ya habari kuwaelimisha wananchi umuhimu wa Katiba inyopendekezwa kabla ya kuipigia kura katiba hiyo.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Asha-Rose Migiro wakati wa hafla fupi ya kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa Taasisi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu.

“Taaluma ya habari ni mhimili wa nne wa serikali, itumieni taaluma hii kuwaelimisha wananchi umuhimu wa katiba inayopendekezwa,” alisema Waziri Migiro.

Waziri Migiro alifafanua kuwa waandishi wa habari ni watu muhimu katika jamii ambao wana uwezo wa kufikisha habari kwa wananchi kwa haraka na kwa wakati hivyo wanatakiwa kutumia fursa  hii kuwaelimisha, kuwajenga na kuwafahamisha wananchi habari mbalimbali zikiwa zile zinazohusu masuala ya katiba.

Akizungumza kuhusu suala la watu wenye ulemavu, Waziri Migiro alisema kuwa watu hao wana haki yao kikatiba, hivyo Serikali imechapisha nakala katika maandishi ya nukta nundu na maandishi makubwa ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata katiba mpya.

“Walemavu wana haki yao kikatiba ndo maana serikali imechapisha nakala za Katiba inayopendekezwa kwa maandishi ya nukta nundu na maandishi makubwa ili nao waweze kusoma na kushiriki katika upigaji kura,” alisema Dokta Migiro.

Waziri Migiro aliongeza kuwa mchakato wa Katiba Inayopendekezwa unamhusu kila Mwananchi, hivyo kutokana na sababu hii, Serikali imesambaza nakala za Katiba Inayopendekezwa moja kwa moja kwa wananchi na sasa hafla hii ni ya kukabishi nakala hizi kwa viongozi wa Taasisi ambao watasambaza kwa taasisi mbalimbali ili waweze  kuzisoma na kuongeza uelewa wa maudhui ya Katiba inayopendekezwa.

Aidha, Waziri Migiro aliwashukuru waalikwa wote kwa umoja na uwingi wao wa kushiriki katika hafla hii ya kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa kwa taasisi mbalimbali na aliwasihi viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha kuwa nakala hizi zinawanufaisha walio chini yao iwezekanavyo.

“Wito wangu kwa viongozi wao ni kuwa wahakikishe nakala hizi zinawanufaisha wenzao wengi iwezekanavyo, “Alisema.

Wiki kadhaa zilizopita, jumla ya nakala milioni 2 za Katiba Inayopendekezwa zimechapishwa na kusambazwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa upande wa Zanzibar, nakala laki mbili  zilisambazwa kwa wananchi kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kwa upande wa Tanzania Bara, jumla ya nakala 1,141,300 zilisambazwa ambapo kila kata imepelekewa nakala mia tatu chini ya uratibu wa uongozi wa mikoa na Wilaya.

-Mwisho-

Matukio Mapya

Hakuna Tukio kwa sasa.

Anuani

KATIBU MKUU

  • Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
  • Barabara ya Mkalama,
  • Jengo la Taaluma Na. 1,
  • Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM,
  • S.L.B. 315,
  • DODOMA.
  • Simu:+255 26 2321680
  • Nukushi: +255 26 2321679
  • Tovuti www.sheria.go.tz
  • Barua pepe: km@sheria.go.tz