Upo Hapa: Home

MPANGO KAZI WA KIKANDA KUDHIBITI DAWA ZA KULEVYA NA MAKOSA MENGINE YA JINAI WAZINDULIWA

E-mail Print PDF

Mataifa 13 ya kanda ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia udhibiti dawa za kulevya na makosa mengine ya jinai (UNODC) yenye makao yake mjini Nairobi, Kenya yamezindua mpango kazi wa kikanda uliobuniwa na mataifa hayo.

Uzinduzi huo pia ulihusisha uwekaji saini Tamko la pamoja la mataifa hayo kuhusu kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza mapambano dhidi ya dawa za kulevya na makosa mengine ambayo ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inawajibika nayo.

Uzinduzi huo uliofanyika tarehe 29 Agosti 2016 jijini Nairobi, Kenya na kuhudhuriwa na nchi za Burundi, Visiwa vya Comoro, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Mauritius, Rwanda, Visiwa vya Shelisheli (Seychelles), Somalia, Uganda na Mataifa hayo, Tanzania ambayo iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria, Prof Sifuni Ernest Mchome.

Akizungumzia mpango kazi uliozinduliwa, Prof. Mchome amesema malengo ya mpango kazi huo yanaenda sambamba na dhamira na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kupambamba na maovu mbalimbali ikiwemo dawa za kulevya, rushwa, usafirishaji haramu wa binadamu na vitendo vya ugaidi na kuongeza kuwa mpango kazi huo piaunaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) 2030 na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 ambayo Tanzania imeshiriki katika uandaaji wake na kuridhia kuutekeleza.

Amesema kama Taifa linalohitaji maendeleo kwa haraka, Tanzania haina budi kuuchangamkia mpango huo ambao siyo tu utasaidia katika kujenga uwezo wa wataalamu wake, taasisi na vyombo mbalimbali vya dola pia utasaidia kubadilishana taarifa mbalimbali kuhusu makosa haya na mwenendo wake kwa ujumla ili kufanikisha azma ya mataifa yote katika eneo hili kuyadhibiti na hatimaye kuyazuia maovu hayo yasiendelee.

Mpango huo umejikita katika nguzo kuu tano ambazo ni udhibiti wa makosa yanayovuka mipaka na usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, binadamu, fedha na makosa mengine ya aina hiyo, udhibiti wa rushwa, kuzuia ugaidi, kuimarisha mifumo ya kuzuia makosa ya jinai na ile ya utoaji haki jinai na udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya, tiba kwa wale walioathirika nazo na udhibiti wa maambukizi ya VVU

Prof Mchome amesema nguzo hizo zimelenga kuunga mkono na kuimarisha uwezo wa mataifa haya kudhibiti na kupambana na vitendo vya aina hiyo, kuimarisha uwezo wa mataifa haya katika utekelezaji wa Mkataba wa Ummoja wa Mataifa Dhidi ya Rushwa, kuunga mkono na kuimarisha mifumo ya kitaifa ya makosa ya jinai ili kuiwezesha kumudu na hivyo kukabiliana ipasavyo na tishio la ugaidi ambao unaendelea kusambaa katika mataifa mbalimbali. Malengo mengine ni kuiwezesha mifumo hiyo kufanya kazi kwa ufanisi, kuzingatia haki, uwajibikaji bila upendeleo kulingana na misingi ya utoaji haki jinai inayotambuliwa na mikataba mbalimbali ya kimataifa na kuwezesha mataifa husika kuwa na mifumo endelevu iliyojengwa katika misingi yenye ushahidi kuhusu udhibiti wa matumizi ya dawa za kulevya na jinsi ya kukabiliana na madhara yake ikiwemo maambukizi ya VVU.

-Mwisho-

Matukio Mapya

Hakuna Tukio kwa sasa.

Anuani

KATIBU MKUU

  • Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
  • Barabara ya Mkalama,
  • Jengo la Taaluma Na. 1,
  • Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM,
  • S.L.B. 315,
  • DODOMA.
  • Simu:+255 26 2321680
  • Nukushi: +255 26 2321679
  • Tovuti www.sheria.go.tz
  • Barua pepe: km@sheria.go.tz