Upo Hapa: Home

MAJALADA 300 YANAFANYIWA TATHMINI KUPELEKWA MBELE YA DIVISHENI MAALUM YA MAHAKAMA.

E-mail Print PDF

 

Majalada 300 yamefikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini –DPP kwa ajili ya kufanyiwa tathmini ili kuhakikisha kuwa ushahidi uliopo ni madhubuti na unajitosheleza, kazi hiyo ikikamilika majalada yatafikishwa mbele ya vyombo vya sheria ikiwemo divisheni maalum ya Mahakama inayoshughulikia makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini kulingana na vigezo vilivyowekwa.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome aliyasema hayo jijini Dar es Salaam kupitia kipindi Maalum cha TV cha TUNATEKELEZA kilichorushwa na Televisheni ya Taifa TBC1 juzi usiku.

Alisema Divisheni hiyo maalum ya Mahakama ipo na ilishaanza kazi tangu Julai 8 mwaka huu kufuatia kutiwa saini kwa Sheria ya kuanzishwa kwake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Divisheni hiyo maalum ya mahakama ipo na ilishaanza kazi, mpaka sasa kuna Mashauri zaidi ya 300 na kitu hivi, ambayo yanachunguzwa, ili kujihakikishia kuwa ushahidi uliopo ni madhubuti na unajitosheleza na kazi hiyo ikikamilika mtaziona katika divisheni hiyo, hatutaki kupeleka mashauri dhaifu pale, ambayo yakipitiwa na majaji husika yatafutwa, tunataka tuwe na uhakika nayo kuwa yakipelekwa huko mashauri hayo kusiwe na mashaka yoyote”, alisema Prof Mchome.

Aliongeza kuwa sheria iliyoanzisha divisheni hiyo maalum ilisema mashauri yote yatakayopelekwa katika mahakama hiyo ni yale yatakayokuwa na kiwango cha kuanzia Shilingi bilioni moja na kuendelea na pia ambayo yatakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa nchi.

Hata hivyo hivyo alisema kuwa taasisi zitakazohusika na kuyafanyia uchunguzi mashauri hayo zinaweza kumshauri Mkurugenzi wa Mashitaka akayapeleka mashauri ambayo yako chini ya kiwango tajwa kwa kuzingatia kile watakachoona wakati wa kuyachunguza mashauri hayo.

Alisema kuwa ana imani sasa vitendo vya uhalifu ambao unaliletea athari kubwa kiuchumi taifa vitapungua kutokana na kutungwa kwa sheria hiyo ya kuanzishwa kwa Mahakama hiyo maalum na hivyo kufanikisha lengo mojawapo la kutunga sheria nchini la kuwafanya watu waogope na kuacha kufanya vitendo vya kihalifu “Sheria lazima ziogopwe, zisipoogopwa utaona vitendo viovu vikishamiri nchini na sheria hiyo lazima irekebishwe ili kuongezewa nguvu, ndio maana siku hizi taarifa za watu kukamatwa na nyara za serikali au rushwa kubwa zimepungua.” alisema.

Kuanzishwa kwa Divisheni hiyo maalum ya mahakama inayoshughulikia makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Chama cha Mapinduzi katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 ambayo pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli aliitoa wakati akifungua Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.

Divisheni hiyo iliyoanza kazi mwezi Julai, inaendesha shughuli zake kwa Kanda ya Mahakama Kuu Dar es salaam katika majengo ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo yaliyoko kando ya barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam na katika kanda nyingine za Mahakama Kuu nchini kote.

-Mwisho-

 

 

 

 

 

Matukio Mapya

Hakuna Tukio kwa sasa.

Anuani

KATIBU MKUU

  • Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
  • Barabara ya Mkalama,
  • Jengo la Taaluma Na. 1,
  • Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM,
  • S.L.B. 315,
  • DODOMA.
  • Simu:+255 26 2321680
  • Nukushi: +255 26 2321679
  • Tovuti www.sheria.go.tz
  • Barua pepe: km@sheria.go.tz