Upo Hapa: Home

SERIKALI YAANZISHA MJADALA KUREKEBISHA SHERIA YA NDOA YA 1971

E-mail Print PDF

 

Serikali imeanza mjadala na baadhi ya wadau ili kupata maoni yao juu ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ili kumlinda mtoto.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao kazi cha kujadili mapendekezo ya kuifanyia marekebisho sheria ya ndoa ya 1971 jijini Dar es salaam Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome amesema serikali imedhamiria kuifanyia marekebisho sheria hiyo ili iende na wakati na kumlinda mtoto wa kike nchini.

“Tumeamua kuifanyia marekebisho sheria hii kutokana na ukweli kwamba jamii na wanaharakati wameizungumza sana, huku mazingira yakiwa yamebadilika , kuridhia mikataba ya kikanda na kimataifa ambayo ina lenga kumlinda mtoto na kufanya Utafiti juu ya mapungufu yaliyomo katika Sheria ya Ndoa kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria. Hili ni suala ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu hadi ikafikia jamii kukosa imani na Serikali,na kutokana na hali hiyo tumeamua kuanza kukaa na baadhi ya wadau ili tuweze kupata maoni juu ya kurekebisha sheria hiyo,” alisema Prof Mchome.

Alisema Serikali imekuwa ikikerwa na suala hilo na kuchukua hatua madhubuti za Kisera na Kisheria kumlinda Mtoto hasa wa Kike kwa kuweka makosa ya kujamiiana (statutory rape) kwa mtoto chini ya mika 18 na kufanya elimu hadi ya Sekondari kuwa ya lazima na kuweka marufuku ya kumuoa/kumuoza mtoto wa kike ambaye bado yuko shuleni, iwe ya Msingi au Sekondari ili aweze kumaliza shule angalau ya Sekondari na kufikia malengo yake ya kimaisha.

“Serikali imechukua hatua madhubuti za Kisera na Kisheria ili kumlinda Mtoto wa Kike dhidi ya ndoa za utotoni kwa kuweka makosa ya kujamiiana (statutory rape) kwa mtoto chini ya mika 18, kKufanya elimu hadi ya Sekondari kuwa ya lazima; na kuweka marufuku ya kumuoa/kumuoza mtoto wa kike ambaye bado yuko shuleni, iwe ya Msingi au Sekondari, nia hapaikiwa ni kumlinda mtoto hususan wa kike ili aweze kumaliza shule angalau Sekondari na kufikia malengo yake ya kimaisha,” alisema

Alisema Serikali ilichelewa kuifanyia marekebisho sheria hiyo kutokana na ukweli kuwa suala la ndoa haligusi sheria pekee, linagusa pia mila, desturi na imani za dini na kuongeza kuwa kwa hali hiyo, haitakuwa busara kwa serikali ambayo inaheshimu imani za kidini na inatambua uwepo wa mila na desturi zinazofuatwa na makabila mbalimbali  na kujichukulia jukumu la kuamua bila ya kupata maoni na ridhaa ya wananchi na kuongeza kuwa sasa serikali inaona ni wakati muafaka kuingia katika mjadala na wadau ili kukamilisha hatua zilizoanza kufanyika kupitia Sera na Sheria nyingine.

Wadau kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia Wanawake-UN-Women, Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia Watoto- UNICEF, wanasheria kutoka WILDAF, WILAC, TAWLA na Wizara ya Mambo ya Katiba Sheria na taasisi zake na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto.

-Mwisho-

Matukio Mapya

Hakuna Tukio kwa sasa.

Anuani

KATIBU MKUU

  • Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
  • Barabara ya Mkalama,
  • Jengo la Taaluma Na. 1,
  • Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM,
  • S.L.B. 315,
  • DODOMA.
  • Simu:+255 26 2321680
  • Nukushi: +255 26 2321679
  • Tovuti www.sheria.go.tz
  • Barua pepe: km@sheria.go.tz