Upo Hapa: Home

SERIKALI YAWASILISHA BUNGENI MSWADA WA SHERIA YA MSAADA WA KISHERIA

E-mail Print PDF

 

Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria iliwasilisha Bungeni Mswada wa Sheria ya Msaada wa Kisheria. Hayo yalisemwa leo na Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mhe.Dkt. Harrison Mwakyembe wakati akiongea na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara.

Waziri Mwakyembe amesema kuwa mswada huo ulisomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10, mwaka huu ukiwa na lengo la kuwa sheria itakayosimamia na kuratibu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za mawakili, kuwatambua wasaidizi wa kisheria (paralegals) pamoja na mambo mengine yanayohusiana na utoaji wa msaada wa kisheria nchini.“Lengo ni kuhakikisha kuwa kila mtu bila kujali kipato chake anapata haki yake katika mamlaka husika za utoaji haki kwa wakati.” Alisema Waziri Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe alisema kuwa mswada huo umepitia ngazi zote za maamuzi ndani ya Serikali  na sasa upo mikononi mwa mamlaka ya Bunge ambao wataweka utaratibu kwa ajili ya wadau kutoa maoni. “Muswada huu kwa sasa upo wazi kwa ajili ya wadau kutoa maoni na Bunge kama chombo pekee kinachohusika na kuratibu na kupokea maoni ya wadau kupitia kamati yake ya Katiba na Sheria kitaweka utaratibu mzuri ili wadau waweze kutoa maoni.” Aliongeza Waziri Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe aliwaomba pia wananchi wote pamoja na wadau wengine kujipatia nakala ya Mswada huu ili wausome kwa makini na hatimaye wapeleke maoni yao kwa Kamati husika ya Bunge wakati utakapowadia. “Ninajua kuwa Bunge litaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kupokea maoni ya wadau wote watakaofika mbele ya kamati lakini pia watakaowasilisha maoni yao kwa wananchi, hivyo ninawasihi wananchi wote wasome msada huu na hatimaye wakati utakapowadia watumie fursa hii kutoa maoni yao.” Alisema Waziri Mwakyembe.

Katika kuelimisha umma, aliwataka waandishi wa Habari kusaidia kusambaza mswada huu kwa kuuchapa katika magazeti ili kila wananchi wapate nafasi ya kuusoma na kuulewa na hatimaye waweze kuutolea maoni vizuri mswada ambao wamekwisha usoma.

Wizara ya Katiba na Sheria mwaka 2012 iliunda chombo cha Sekretarieti ya Msaada wa Kisheria  kijulikanacho kwa jina la kiingereza Legal Aid Secretariat (LAS) kikiwa na lengo la kuratibu shuguhuli za utoaji wa Msaada wa Kisheria hapa nchini. Chombo hicho ndicho kilichopewa mamlaka ya kuratibu watoa msaada wa kisheria wanaotambulika kwa jina la Legal Aid Providers (LAPs) ambao wanajumuisha Taasisi na Mashirika yote yasiyo ya Kiserikali, Vyama vya Wanasheria pamoja na Wasaidizi wa Kisheria(Paralegal Units).

-Mwisho-

Matukio Mapya

Hakuna Tukio kwa sasa.

Anuani

KATIBU MKUU

  • Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria,
  • Barabara ya Mkalama,
  • Jengo la Taaluma Na. 1,
  • Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria cha Chuo Kikuu cha Dodoma- UDOM,
  • S.L.B. 315,
  • DODOMA.
  • Simu:+255 26 2321680
  • Nukushi: +255 26 2321679
  • Tovuti www.sheria.go.tz
  • Barua pepe: km@sheria.go.tz